Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleimani Jafo ameutaka uongozi wa shule za Sekondari kuhakikisha unadhibiti wanafunzi wasiwe na simu za mikononi wawapo shuleni.
Akizungumza jana wakati wa ukaguzi wa ukarabati wa shule ya Sekondari ya Bweni ya Ruvu iliyokoko mkoani Pwani, Waziri Jafo ameagiza wanafunzi hao kudhibitiwa wasiwe na simu za mkononi shuleni kwani hutumia muda wao mwingi katika kufuatilia masuala yasiyo na tija kwenye masomo yao.
“Unakuta wanafunzi wengi hawafuatilii masomo, wao ni kushinda mitandaoni wanachati kwenye mitandao ya kijamii kama Instagram,” alisema Jafo.
Katika hatua nyingine, Waziri Jafo alimtaka atakayekabidhiwa jukumu la kufanya ukarabati wa shule hiyo aikamilishe kwa muda ili kuboresha mazingira ya shule hiyo kongwe.
Alisema kuwa ukarabati wa shule hiyo ni sehemu ya hatua za Serikali kuhakikisha inakarabati shule zote kongwe nchini ili kuboresha zaidi mazingira ya utoaji elimu.
Aliongeza kuwa atahakikisha anashirikiana na mbunge wa jimbo hilo, Hamood Abuu kufuatilia kwa ukaribu hatua zote za ukarabati wa shule hiyo.
Jafo ameendelea kuzulu shule za Sekondari, ikiwa ni siku chache tangu aizulu shule ya Sekondari ya Wasichana ya Jangwani ambapo alimuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam kubadili uongozi wa shule hiyo mara moja, kufuatia shule hiyo kufanya vibaya kwenye mitihani ya Taifa (Necta).