Mwenyekiti wa Tume Ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Damian Lubuva, amesema kuwa Tume hiyo imenza kuchoshwa na matamko yanayotolewa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Jaji Lubuva ameeleza hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa anaongea na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari.

Alisema kuwa malalamiko ya Chadema yamekuwa hayana msingi huku akiwataka viongozi wa chama hicho kukaa kimya na kusubiri Oktoba 25, kama hawana vitu vya msingi vya kuzungumza kwenye mikutano yao.

“Tumeanza kuchoshwa na kauli hizi za kusema Tume imeshindwa kudhibiti wizi wa kura, ikiwa wanajua namna kura zinavyoibiwa watuelekeze dirisha hili ili tukanunue saruji na nondo tulizibe, sisi katika NEC msamiati wa kubariki bao la mkono haupo,” alisema Jaji Lubuva.

Alisisitza kuwa Tume haitambui msemo wa ‘bao la mkono’ uliotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, aliyesema kuwa Chama chake kitashinda hata kwa ‘bao la mkono’. Kauli inayotafsiriwa kama kushinda hata kwa njia zisizo halali.

“Wanaosema watagomea matokeo ya uchaguzi baada ya kushindwa wajue wanakwenda kinyume na maadili ya uchaguzi, kauli hizo zinatoa taswira za kuichokoza Tume. Hata katika mpira wa miguu bao la mkono haliruhisiwi, hakuna njia ya mkato ya kushinda uchaguzi,” alisema.

Tanzia: Askari Wa JWTZ Wapotea Baharini, Wengine Wafariki Kwa Ajali Ya Basi
Lowassa Atangaza Neema Ya Siku 100 Za Serikali Yake