Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahimu Juma amewataka viongozi wa serikali na vyama vya siasa kuacha mara moja vitendo vya kuingilia mhimili wa Mahakama na kuvunja amri zake.
Ameyasema hayo leo Jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wiki ya Sheria inayotarajiwa kufanyika mwanzoni mwa mwezi ujao (Februari mosi).
“Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania mamlaka ya utoaji haki ni ya Mahakama tu, nawasihi viongozi wote wa serikali wenye mamlaka za kikatiba na kisheria wabaki ndani ya maeneo yao ya Kikatiba na wajiepushe kuingilia maeneo yaliyo ndani ya haki, hadhi na Mamlaka ya Kikatiba ya Mahakama,” amesema Jaji Prof. Juma
Hata hivyo, ametoa rai kwa wananchi na wadau wote wa sheria kutembelea Mnazi Mmoja kwa ajili ya kujifunza na kupata huduma mbalimbali za Kisheria kutoka kwa Majaji, Mahakimu, Wasajili, Watendaji, Mawakili wa serikali na Mawakili wanaojitegemea ambao watakuwa tayari kuwasikiliza na kuwahudumia.