Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma amesema, kati ya kesi za jinai 100 zilizofikishwa katika mahakama ya wilaya Namtumbo mkoani Ruvuma kuanzia mwezi Julai 2021 hadi Januari mwaka 2022, 44 zimeshindwa kusikilizwa kutokana na upelelezi wake kushindwa kukamilika.
Prof. Juma amesema hayo,wakati akizungumza na Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Dkt Julius Ningu alipotembelea wilaya hiyo kukagua ujenzi wa jengo la mahakama na kuzungumza na watumishi kwa lengo la kuhimiza na kukumbusha kufanya kazi kwa misingi ya ukweli na weledi wanapotekeleza majukumu yao.
Aidha amefafanua kuwa,kwa kawaida mashauri au kesi zinazofunguliwa katika mahakama ya mwanzo zinatakiwa zisikae bila kusikilizwa zaidi ya miezi sita,mahakama ya wilaya miezi 12 na mahakama kuu miezi 24,lakini katika wilaya hiyo kesi zilizokwama katika mahakama ya wilaya zimevuka muda wa kesi za mahakama kuu.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu asilimia 80 ya kesi za jinai zilizokaa bila kusikilizwa, mahakama ya wilaya ya Namtumbo haina mamlaka ya kusikiliza kwa sababu ya kutokamilika kwa upelelezi na uendeshaji wa mashauri husika.
Alisema, adhima ya mahakama Tanzania ni kuhakikisha kesi na mashauri yote yanayofikishwa mahakamani yanasikilizwa na kutolewa hukumu haraka badala ya kukaa muda mrefu.
Amewaomba wadau wakiwamo Jeshi la Polisi, kuharakisha upelelezi ili kesi zimalizike kwa wakati na kuepuka kukaa muda mrefu na kusababisha mlundikano wa mahabusu gerezani na malalamiko ya wananchi.
Akizungumza na watumishi wa mahakama Jaji Mkuu alisema,licha ya maboresha makubwa yaliyofanywa lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanya katika baadhi ya maeneo kutokana na uchafu wa miundombinu ya mahakama.
Alisema, kuanzia sasa ni muhimu kwa mahakama kutenga bajeti kwa ajili ya kuendesha na kuendelea kuboresha miundombinu ili shughuli za mahakama ziweze kufanyika na watumishi kufanya kazi kwa weledi.
Amewapongeza watumishi wa wilaya hiyo kwa jitihada ambazo zimesaidia kupunguza malalamiko ya wananchi,hata hivyo amewataka kutoa huduma bora ili watu wanaofika mahakamani waione mahakama ni chombo sahihi kinachotoa haki.
Alisema,mahakama imeanza kufanya maboresho mbalimbali ambayo yameonesha matokeo mazuri kwa wananchi kuamini kuwa mahakama ni chombo chao,hivyo ni muhimu kuwa na watumishi wakweli,wanaofuata maadili na kutumia weledi wanaposikiliza mashauri mahakamani.
Naye Mkuu wa wilaya hiyo Dkt Julius Ningu ameipongeza mahakama kwa kufanya maboresho makubwa ya kiutendaji na miundombinu yake katika kipindi kifupi.
Alisema,hapo mwanzo mtu akipata wito wa mahakamani jambo analofikiria anakwenda kuhukumiwa, hali hiyo ilisababisha wananchi wengi kushindwa kutokea mahakamani hata kama ameitwa kwa ajili ya kutoa ushahidi.
Naye Hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya Namtumbo Glory Lwobile alitaja changamoto kubwa ni ufinyu wa bajeti ambayo imechangia sana kutosikilizwa kwa baadhi ya mashauri hasa makosa ya uhujumu uchumi.
Alisema, hali hiyo inasababisha mashaidi kukataa kufika mahakamani kwa kuhofia kutopewa nauli ya kwenda mahakamani na kurudi katika maeneo yao.