Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla za uzinduzi wa Mahakama ya Wilaya ya Same na Mwanga, mkoani Kilimanjarotarehe 15 Novemba, 2022 katika jengo jipya la Mahakama ya Wilaya ya Mwanga.
Uzinduzi huu ni mwanzo wa uzinduzi wa miradi mingine 24 ya Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya itakayozinduliwa mwezi huu Novemba na mwezi Disemba mwaka huu 2022.
Miradi hii miwili iliyopo mkoani Kilimanjaro imeanza kutumika na inatarajiwa kuwezesha watumishi wa Wilaya hizo kuwa katika majengo yatakayokuwa na mzingira rafiki ya utoaji wa huduma kwa wananchi zaidi kwa kutumia mfumo ya kitekinolojia.
Ujenzi wa miradi hii imezingatia mahitaji ya kisasa ya wadau wa mnyororo wa utoaji haki ambapo kutakuwa na ofisi za Mawakili, Maafisa Magereza, Ustawi wa Jamii na watu wenye mahitaji maalum na watoto wamewekewa vyumba vya kutumia wakiwa mahakamani hapo.
Miradi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama wa Miaka mitano (5) wa 2020/21-2024/25 katika nguzo ya upatikanaji wa haki kwa wakati kupitia uboreshaji wa miundombinu ya majengo na kusogeza huduma za haki karibu na wananchi.
Halfa ya uzinduzi inatarajiwa kuhudhuriwa na Viongozi Waandamizi wa Mahakama na Serikali wakiwemo Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mustapher Siyani, Msajili Mkuu wa Mahakama Wilbert Chuma, Waziri wa Fedha na Uchumi, Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumaro, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu na Wabunge toka majimbo ya Mkoa wa Kilimanjaro.
Wananchi wa Wilaya ya Mwanga na Same wanaombwa kujitokeza katika Viwanja vya Mahakama ya Wilaya ya Mwanga kushuhudia uzinduzi huo ambao ni ishara ya kuwepo mabadiliko makubwa ya maboresho ya utoaji huduma za Mahakama nchini.