Siku chache baada ya vyama vya upinzani vya Chadema na CUF (Upande wa Profesa Ibrahim Lipumba) kutishiana kuharibiana kupitia oparesheni zao mpya, msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amevionya vyama hivyo.

Chadema walikuwa wa kwanza kutangaza kuingilia mgogoro ndani ya CUF wakitangaza kuanzisha ‘Oparesheni Ondoa Msaliti Buguruni’ wakilenga kumuondoa mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na ofisi ya Msajili, Profesa Ibrahim Lipumba.

CUF inayomuunga mkono Profesa Lipumba pia ilijibu mapigo kwa kudai kuwa itakuja na ‘Oparesheni Futa Chadema’, wakilaani kitendo cha Chadema kuingilia mgogoro huo.

Kufuatia kauli hizo, Jaji Mutungi amevionya vyama hivyo kuwa vitakabiliwa na mkono wa sheria endapo vitajihusisha na vurugu ya aina yoyote.

Msajili aliongeza kuwa ingawa amesikia kupitia vyombo vya habari vitisho hivyo, hajapokea barua yoyote ya malalamiko ofisini kwake kutoka kwa vyama hivyo.

“Natoa onyo kwa chama chochote cha siasa ambacho kitaonesha ubabe na kutumia wafuasi wake waweze kufanya vurugu. Tutakichukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria,” Jaji Mutungi anakaririwa na Mtanzania.

“Kama kungekuwa na tatizo wangeleta barua ofisini kwangu ya malalamiko, lakini mpaka sasa sijapata barua yoyote inayohusiana na madai yao zaidi ya kusoma kwenye vyombo vya habari,” aliongeza.

Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea alifanya mkutano na vyombo vya habari hivi karibuni jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa wamebaini Profesa Lipumba anatumika kuidhoofisha CUF hali itakayodhoofisha pia muungano wa Ukawa, hivyo wameamua kumuunga mkono Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad. Kubenea alitangaza rasmi ‘Oparesheni Ondoa Msaliti Buguruni’ akidai kuwa tayari ilishaanza wakiwa Bungeni mjini Dodoma kwa kuwatenga wote wanaoshirikiana na Profesa Lipumba.

Saa chache baadae, Naibu Katibu Mkuu CUF upande wa Bara, Magdalena Sakaya ambaye anatambuliwa na Ofisi ya Msajili na anayemuunga mkono Profesa Lipumba alijibu mapigo kwa kueleza kuwa kambi yake itakuja na ‘Oparesheni Futa Chadema’.

Video: Lowassa apewa saa 168, Mtikisiko Acacia
Magazeti ya Tanzania leo Julai 14, 2017