Rais mstaafu wa awamu ya nne, Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete, ameipongeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, kutumia Tamasha la 40 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo kutoa huduma ya ushauri na kuchanja ugonjwa wa Uviko -19 na kupima UKIMWI kwa hiari kwenye Tamasha hilo.
Kikwete ametoa pongezi hizo wakati akihitimisha tamasha hilo ambapo amefafanua umuhimu wa sekta hizo kwa Taifa, amesema kutokana na umuhimu wa Sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo, haijawahi kutokea kuachwa kuundwa Wizara katika awamu zote toka enzi ya Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Nyerere na kwamba kutokana na umuhimu huo Rais Samia ameendelea kuzibakiza na kuziboresha.
“Wizara iliundwa kuukuza utamaduni wetu na utamaduni wetu ndiyo kielelezo cha Mtanzania,” Amesema Dkt. Kikwete
Aidha ameipongeza Wizara kwa kuendelea kuboresha sekta za Sanaa na Utamaduni kupitia taasisi zake za Bodi ya Filamu, COSOTA, BASATA na BAKITA na kuzitaka ziendelee kusimamia na kusaidia kazi za Wasanii ili waweze kunufaika nazo.
“Nimefurahi kuona siku hizi mnawatengenezea Wasanii mazingira bora zaidi hivyo watafaidi matunda ya kazi zao”. Ameongeza Dkt Kikwete.
Katika hatua nyingine Dkt Kikwete amempongeza Rais Samia kwa kutambua na kuthamini kazi nzuri ya kutwaa Kombe la COSAFA iliyofanywa na Timu ya Taifa ya Wanawake ya Mpira wa Miguu (Twiga Stars)
Siku ya mwisho ya Tamasha la Bagamoyo ilikuwa ni maalum kwa ajili ya Muziki wa Singeli ambao amesema yeye ni miongoni mwa wapenzi wa muziki huo wenye asili ya utamaduni wa nchi yetu.