Kuna uwezekano mkubwa kwa mshambuliaji wa KRC Genk pamoja na timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Mbwana Ally Samatta akaondoka nchini Ubelgiji wakati wa usajili wa majira ya kiangazi na kuelekea kwingineko barani Ulaya.
Hayo yamesemwa na meneja wa mshambuliaji huyo Jamal Kisongo alipozungumza na Dar24, kufuatia tetesi zinaendelea kumuandama Mbwana Samatta hasa wakati huu ambao klabu yake inafanya vyema ndani na nje ya Ubelgiji.
Kisongo amesema kiwango cha Mbwana Samatta kimekua kinaendelea kuwa lulu barani Ulaya, na tayari kuna baadhi ya klabu kubwa barani humo zimeonyesha nia ya kuingia vitani kuiwania saini yake.
“Nimesikia na kuona taarifa zinazomuhusu Mbwana kutakiwa nchini Uturuki, lakini ninakuhakikishia hakuna ukweli wa jambo hili, japo kwa sasa ni wakati wa vyombo vya habari kuibua tetesi nyingi kuhusu usajili wa wachezaji,”
“Mbwana ana kiwango kizuri na kinaendelea kukua siku hadi siku, watu wengi wanamfuatilia na wakati mwingine watu hunipigia simu kutoka Ulaya kuhusu mustakabali wake, lakini huwa nawajibu suala moja tu, kuhusu mkataba wa mbwana na klabu yake ya Genk.” Amesema Jamal Kisongo.
Hata hivyo Kisongo amesisitiza kuwa Mbwana Samatta ana kila sababu ya kuondoka nchini Ubelgiji mwishoni mwa msimu huu japo hakuwa tayari kuweka wazi ni wapi atakapoelekea.
Amesema kwa sasa ni vigumu kueleza mustakabali wa mchezaji huyo, kutokana na kutaka kumpa nafasi ya kuelekeza akili yake katika kuisaidia timu yake kufanya vizuri ndani na nje ya Ubelgiji.