Gwiji wa Klabu ya Liverpool Jamie Carragher amesema Mohamed Salah ataingia kwenye kikosi bora cha klabu hiyo cha muda wote baada ya kufikisha mabao 100.
Salah alifikisha idadi hiyo ya mabao baada ya kufunga bao pekee kwenye mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Brenford Jumamosi (Mei 06).
Kocha Jurgen Klopp ameendelea kuiweka Liverpool kwenye nafasi nzuri ya kufuzu Ligi Mabingwa Ulaya msimu ujao baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Brentford.
Bao la Salah dhidi ya Brentford linakuwa la 30 katika mashindano yote aliyocheza msimu huu licha ya Liverpool kusuasua huku Carragher akimsifia.
Akizungumza kupitia kituo cha televisheni cha Sky Sports, amesema Salah atakuwa miongoni ya wachezaji bora wa Liverpool waliowahi kupita Anfield kutokana na mchango mkubwa klabuni hapo.
“Liverpool ina bahati ya kuwa na mchezaji kama Salah, endapo Salah ataondoka jina lake litatukuzwa na mashabiki, nadhani anaingia kwenye kikosi bora cha mastaa wa muda wote, sidhani kama kiwango chake kitashuka, ataendelea kufunga mabao kila msimu,” amesema Carragher.
Vile vile mkongwe huyo aliyewahi kukipiga Liverpool amemsifia Salah akidai kiwango chake kimeendela kuwa imara licha ya Liverpool kupitia kipindi kigumu msimu huu.
“Amekuwa mchezaji bora wa Liverpool, kiwango cha Salah hakijashuka. Ameendelea kuwa bora kila msimu haijalishi kama timu inafanya vizuri au vibaya, ushindi dhidi ya Brentford unaipa Liverpool mwanga wa matumaini,” Carragher ameongeza.