Mshambuliaji wa klabu ya Hibernian Jamie Maclaren amepata bahati ya kuitwa kwa mara ya pili katika kikosi cha timu ya taifa ya Australia, kuchukua nafasi ya mshambuliaji wa klabu ya FC Luzern Tomi Juric ambaye afya yake inaendelea kutia mashaka.
Maclaren alikua miongoni mwa wachezaji waliopunguzwa kwenye kikosi cha Australia kilichokua na wachezaji 32 na kufikia wachezaji 26 mwanzoni mwa mwezi huu, baada ya kuingia kambini mjini Antalya nchini Turkey kwa siku kadhaa.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 24, aetolewa kwa mkopo nchini Scotland akitokea Ujerumani kwenye klabu ya daraja la pili ya Darmstadt 98, alirejea kambini jana jumapili, tayari kwa maandalizi ya mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Jamuhuri ya Czech Republic utakaochezwa nchini Austria Juni mosi.
“Tomi Juric anasumbuliwa na majeraha ya goti kwa zaidi ya majuma matatu sasa, amekua akifuatiliwa kwa ukaribu na jopo la madaktari wa timu,” amesema kocha wa Australia van Marwijk.
Tomi Juric
“Tunatarajia Tomi huenda akawa FIT na kucheza tena ndani ya majuma kadhaa yajayo, lakini kupona kwake hakutoweza kuisaidia timu itakapokua Urusi ikishiriki fainali za kombe la dunia.
“Hivyo nimeamua kumrudisha kikosini Jamie Maclaren, ambapo ninaamini ataweza kuziba nafasi ya Tomi kikamilifu kwa kuonyesha uwezo wake na kuwa ndani ya kikosi cha wachezaji 23 nitakachokitangaza siku za usoni.”
Australia pamoja na matafa mengine shiriki, itatakiwa kuwasilisha orodha ya wachezaji 23 hadi Juni 04, tayari kwa ushiriki wa fainali hizo ambazo zitaanza rasmi Juni 14.
Hata hivyo kikosi cha mwisho cha wachezaji 23 cha Australia kinatarajiwa kucheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Hungary mjini Budapest Juni 09.
Australia wamepangwa katika kundi C, lenye timu za Denmark, Peru na mabingwa wa dunia wa mwaka 1998 timu ya taifa ya Ufaransa.