Serikali imewataka Viongozi na wananchi wote kutumia vizuri mvua zinazoendelea kunyesha nchini kwa ajili ya shughuli za uzalishaji mali.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Watu Wenye Ulemavu, Stella Ikupa wakati akizungumza na waandishi wa habari juu tahadhari kwa umma kuhusu mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema kuwa, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ilitoa utabiri wa msimu wa mvua za vuli kwa kipindi cha mwezi Oktoba mpaka Desemba 2017 kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua.

Aidha, ameongeza kuwa kutokana na taarifa hiyo serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ilielekeza Wizara na mamlaka za Serikali za Mitaa kuchukua hatua stahiki kwa kutumia mvua hizo kwa shughuli za uzalishaji mali pamoja na na kuchukua hatua za tahadhari kwa madhara yanayoweza kujitokeza.

“Kamati za usimamizi wa Maafa kuanzia ngazi ya kijiji na mitaa zinatakiwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa namba 7 ya mwaka 2015 na kanuni za usimamizi wa maafa za mwaka 2017 ya kuchukua hatua za kuzuia, kupunguza madhara na kujiandaa kukabiliana na maafa endapo yatatokea,” amesema Ikupa.

Hata hivyo, ameongeza kuwa mvua hizo zinaendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini na tayari baadhi ya maeneo yaliyotabiriwa kupata mvua nyingi yameanza kupata madhara mbalimbali yaliyosababishwa na mafuriko vikiwemo vifo, magonjwa ya milipuko, uharibifu wa mazao mashambani, uharibifu wa mazingira, mali na miundombinu.

 

Mbali na hayo, amesema kuwa Serikali itaendelea kutoa tahadhari za mara kwa mara kupitia vyombo vya habari kadri ya hali inavyojitokeza, hivyo wananchi mnaombwa kufuatilia kwa makini na kuchukua hatua stahiki

Kama ulituma Waraka huu imekula kwako
TFF kula sahani moja na waliosambaza ujumbe batili