Klabu ya Chelsea imeendelea kukumbwa na janga la majeraha kwa wachezaji wake sambamba na mwenendo mbovu kwenye Ligi Kuu England ambako imeshinda mara moja katika mechi sita.

Chelsea imepata pigo jingine baada ya beki wake tegemeo Benjamin James Chilwell kuumia wakati wa mechi ya raundi tatu va Kombe la Carabao dhidi ya Brighton.

Kuna uwezekano mkubwa beki huyo kutoka England, akakosa mechi inayofuata ya Ligi Kuu England dhidi ya Fulham ambayo itachezwa Jumatatu (Oktoba 02).

Chilwell ameumia siku chache tu baada ya nahodha wa timu hiyo Reece James kuondolewa kikosini baada ya kuumia, hali ambayo inampa wakati mgumu kocha Mauricio Pochettino ambaye bado anajenga kikosi chake.

Akithibitisha kuhusu hali ya beki huyo Pochettio alisema: “Chilwell ameumia ni kweli, tutamuangalia lakini nadhani ni maumivu ya misuli.”

Mpaka sasa Chelsea ina wachezaji majeruhi saba akiwamo Christopher Nkunku na Romeo Lavia ambao walisajiliwa hivi karibuni kwenye dirisha la kiangazi.

Aidha, Pochetino ameahidi kwamba mambo yatakuwa sawa licha ya timu hiyo kujikita katika nafasi ya 14 kwenye msinmamo wa Ligi Kuu England.

The Blues ilipokea kichapo cha tatu kwenye Ligi Kuu England dhidi ya Aston Villa mwishoni mwa juma lililopita, lakini kocha huyo amewatuliza mashabiki kutokana na mwenendo mbovu wa timu yao.

Chelsea imekusanya pointi tano tu katika mechi sita za kwanza za Ligi Kuu England, huku ushindi wao pekee waliopata msimu huu waliwafunga Luton Town kabla ya kupisha mechi za kimataifa.

Mabingwa hao wa Ulaya wa mwaka 2021, msimu huu hawapo kwenye michuano yoyote ya Ulaya baada ya kumaliza Ligi Kuu England ya msimu uliopita kwenye nafasi ya 12.

Kocha Al Merreikh atamba kupindua matokeo
Ahmed Ally: Tunafunga hesabu mapema