Uongozi wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Simba SC umeweka wazi utaratibu wao mpya wa usajili hautoi nafasi kwa kocha kuwa mtu wa mwisho kutoa maamuzi ya usajili kutokana na ‘janja janja’ ya baadhi ya mawakala.
Utaratibu huo mpya ndani ya Simba SC, umeanikwa hadharani na mshauri wa masuala ya michezo wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba SC Crescentius Magori alipohojiwa na Azam TV kupitia kipindi cha ‘KUSARA ZA MWISHO’ cha mwishoni mwa juma lililopita.
Magori alisema: “Unajua soka sasa hivi limebadilika sana, sisi Simba tumeweka utaratibu wetu ambapo kocha si mtu wa mwisho wa usajili na tuna sababu zetu,” alisema Magori.
“Soka sasa hivi ni biashara, mawakala wanaokuwa na makocha ndio hao hao pia wanakuwa na wachezaji, ukimpa nafasi ya mwisho kocha kusajili anaweza akaleta wachezaji anaotoka nao kwa wakala mmoja na wasiwe na ubora ila tu wanataka kufanya biashara,”
“Bahati mbaya sana makocha hawakai sana na timu anaweza akaleta wachezaji tukampa mkataba wa miaka miwili kumbe hana uwezo na baadaye kocha anaondoka anatuachia mzigo wa wachezaji wasiokuwa na msaada, sisi Simba tumeligundua hili na ndio maana tuna utaratibu wetu kwenye usajili”.
Alisema miaka ya nyuma kuna timu zilijikuta zikiwa na wachezaji ambao hawakuwa na uwezo, lakini walisajili kwa shinikizo la makocha ili kufanya biashara za mawakala wao.