Mamlaka ya udhibiti wa Usafiri wa ardhini LATRA imetangaza kuanza kwa matumizi ya tiketi za kieletroniki kwenye mabasi yanayokwenda mikoani ambapo Januari 6, 2021 itakuwa mwisho wa kukata tiketi za mkono.
LATRA imesema kuwa watakaoshindwa kufuata huduma hiyo inawapasa kusitisha kutoa huduma kabla ya kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Wakielezea miongoni mwa umuhimu wa kutumia mfumo huo, LATRA wamesema kupitia mfumo huo wananchi watatumia simu kukata tiketi jambo ambalo litaepusha wizi, ulanguzi wa tiketi na adha za wapiga debe.
Sambamba na hilo mfumo huo pia utasaidia kukomesha vitendo vya upandishaji holela wa nauli hasa kipindi cha mwisho wa mwaka.
Maamuzi ya mfumo yanasimamiwa na kanuni ya 4 (2) (c) na leseni ya kusafirisha abiria itatolewa kwa muombaji aliyesajiliwa kwenye mfumo wa tiketi za kieletroniki ulioidhinishwa na mamlaka.
Pia kanuni ya 24(b)(d) inamtaka msafirishaji mwenye leseni ya kusafirisha abiria wa masafa marefu ahakikishe anatoa tiketi za kieletroniki kwa abiria.