Waziri wa Fedha wa Japan Suzuki Shunichi, amesema Serikali ya Japan itaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha inafikia dira yake ya maendeleo kwa ajili ya Watanzania.

Waziri Suzuki ameyasema hayo leo Disemba 27, 2021 aliPokutana na Balozi wa Tanzania nchini Japan Baraka Haran Luvanda kabla ya kuwasilisha hati za utambulisho kwa Mfalme Naruhito, ambapo pamoja na mambo mengine Balozi Luvanda, ameishukuru Japan kwa misaada na mikopo yenye masharti nafuu ya kimaendeleo inayotolewa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha Balozi Luvanda amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Mtukufu Mfalme Naruhito wa Japan leo Disemba 27, 2021 katika Kasri la Mfalme huyo jijini Tokyo.

Mara baada ya Mtukufu Mfalme Naruhito kupokea hati za utambulisho kutoka kwa Balozi Luvanda, amempongeza kwa kuteuliwa katika nafasi hiyo na kumtakia majukumu mema katika kusimamia mahusiano mazuri yaliyojengeka kwa miaka mingi kati ya Japan na Tanzania.

Pia Mfalme Naruhito amemshukuru Balozi Luvanda kwa kumfikishia salamu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Kadhalika, Mfalme Naruhito amemtaka Balozi Luvanda kutembelea maeneo mbalimbali ya Japan kwa lengo la kutafuta fursa za ushirikiano wa kimaendeleo, hususan pale janga la UVIKO-19 litakapokuwa limedhibitiwa.

Rais Samia afanya uteuzi
Rais Farmajo amsimamisha kazi Waziri Mkuu