Uwanja Japoma uliopo mjini Douala nchini Cameroon, utakuwa mwenyeji wa mchezo wa fainali wa ligi ya mabingwa barani Afrika, ambao umepangwa kuchezwa Mei 29 mwaka huu.
Shirikisho la soka barani Afrika (CAF) limethibitisha taarifa za mchezo huo kuchezwa kwenye uwanja huo mpya, leo jumatatu.
Hii itakua ni mara ya kwanza kwa mchezo wa fainali wa ligi ya mabingwa barani Afrika kuchezwa kwenye uwanja mmoja, tofauti na ilivyokua zamani, ambapo timu zilizoingia hatua hiyo zilikua zikicheza kwa mfumo wa nyumbani na ugenini.
Uwanja wa Japoma umetangazwa kuwa mwenyeji wa mchezo wa fainali, baada ya kushindanishwa na uwanja wa Mohammed V uliopo mjini Casablanca, Morocco na Stade Olympique de Radès ulipo Tunisia.
Mshindi wa michezo ya nusu fainali ya ligi ya mabingwa barani Afrika kati ya Raja Casablanca (Morocco) Vs Zamalek (Misri) atapambana na mshindi wa nusu fainali ya pili kati ya Wydad Casablanca (Morocco) Vs Al Ahly (Misri), kwenye hatua ya fainali mjini Douala.
Uwanja wa Prince Moulay Abdellah Sports
CAF pia wamethibitisha mchezo wa fainali wa michuano ya kombe la shirikisho utachezwa kwenye uwanja wa Prince Moulay Abdellah Sports uliopo mjini Rabat, Morocco Mei 24.
Mshindi wa michezo ya nusu fainali ya michuano hiyo kati ya Pyramids FC (Misri) Vs Horoya (Guinea) atacheza na mshindi wa nusu fainali ya pili kati ya RS Berkane Vs Hassania Agadir zote za Morocco, kwenye hatua ya fainali mjini Rabat.