Jay Z ndiye rapa wa kwanza duniani kuwa bilionea, kwa mujibu wa ripoti ya Jarida la Forbes iliyowekwa wazi wiki hii.
Rapa huyo ambaye ni moja kati ya wafanyabiashara wakubwa ametajwa kuufikia ubilionea kupitia biashara zake za muziki pamoja na uwekezaji katika sekta nyingine.
“Katika kipindi cha chini ya muongo mmoja, Jay Z amekusanya ukwasi ambao unakamilisha jumla ya $1 bilioni, hali inayomfanya kuwa mwana hip-hop wa kwanza kufikia kiwango hicho cha utajiri,” ameandika Zack O’Malley, mwandishi wa Jarida la Forbes.
Jarida hilo limetaja vyanzo vya mapato vya rapa huyo mkongwe kuwa ni pamoja na kuwa na hisa ya $70 milioni kwenye kampuni ya usafiri ya Uber, $70 milioni kwenye masuala ya sanaa, $50 milioni kwenye umiliki wa majumba ya kupangisha na muziki, umiliki wa ‘Tidal’ inayouza nyimbo mtandaoni pamoja na umiliki wa Kampuni ya Roc Nation.
Jay Z alizaliwa katika mitaa ya Brooklyn nchini Marekani na kuishi maisha ya shida akilelewa na mama yake. Aliingia rasmi kwenye ramani ya muziki mwaka 1996 alipoachia albam yake ya kwanza ‘Reasonable Doubt’.
Mapema mwaka huu, albam yake ya sita aliyoitoa mwaka 2001 ya ‘The Blue Print’ iliwekwa kwenye Maktaba ya Taifa hilo ikitajwa kuwa miongoni mwa albam zinazostahili kuwa za kihistoria na zenye faida halisi kwenye jamii.
Jigga amemuoa mwanamuziki Beyonce na wamebarikiwa kuwa na watoto watatu.
Mwaka 2004, Dr. Dre alitajwa kuwa ndiye mwanamuziki wa kwanza kuwa bilionea, akitajwa kuwa angeingiza $1.1 bilioni kupitia mauzo ya headphone zake za ‘Beatz by Dre’ kwa kampuni ya Apple.
Hata hivyo, baada ya mahesabu ya makato mbalimbali, kipato chake halisi kilibainika kuwa chini ya $1 bilioni na kumuondoa kwenye orodha hiyo ya kihistoria.