Mwanamke wa kwanza jijini London nchini Uingereza kushtakiwa kwa kosa la kumkeketa mwanaye wa kike mwenye miaka mitatu tu, amehukumiwa kifungo cha miaka 11 jela.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Jaji ambaye alikielezea kitendo hicho kuwa ni kosa kubwa la jinai na unyama.
“Hebu tuweni wawazi, ukeketaji ni aina ya ukatili kwa watoto,” alisema Jaji Philippa Whipple. “Ni kitendo cha kinyama na kosa kubwa la jinai,” aliongeza.
Alisema kuwa hukumu hiyo kwa mwanamke huyo mwenye watoto wawili ni ujumbe kwa watu wote wanaojihusisha na vitendo hivyo kuacha mara moja.
Jaji alimwambia mwanamke huyo ambaye jina lake halitajwi kwa sababu maalum, “kama mama yake mzazi, umesaliti uaminifu wako kwake kama mlinzi wake. Umemsababishia tatizo kubwa la kisaikolojia litakalodumu kwa maisha yake yote.”
Akizungumzia hukumu hiyo, waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza, Sajid Javid aliweka ujumbe kwenye mtandao wa Twitter akieleza kuwa hukumu hiyo ilikuwa ujumbe muhimu katika siku ya wanawake kuwa utatili wa aina yoyote hauvumiliki.
“Ni ujumbe mzuri wa kukumbusha, katika siku ya wanawake duniani, kwamba hatutavumilia vitendo vyovyote vya kinyama,” tafsiri ya tweet ya Waziri Javid.
Kiwango cha juu cha hukumu dhidi ya mtu aliyejihusisha na ukeketaji ni miaka 14 jela. Mwanamke huyo amehukumiwa ikiwa ni miaka 30 tangu sheria ya kupiga marufuku ukeketaji kupitishwa rasmi.