Mahakama ya Wilaya Uvinza mkoani Kigoma imemuhukumu mshitakiwa Jeremia Ngendabanka (31), mkulima, mkazi wa Kijiji cha Buhingu wilayani Uvinza, kwenda jela miaka 20 baada kumtia hatiani kwa kosa la kupatikana na nyara za Serikali.
Mshtakiwa huyo, anadaiwa kutenda kosa hilo Septemba 22, 2022 baada ya kupatikana nyara za Serikali mkono mmoja wa sokwe mtu, kichwa kimoja cha sokwe mtu na ngozi moja ya sokwe mtu vyenye thamani ya shilingi12,056,304.
Akitoa hukumu hiyo Novemba 23, 2023 Hakimu Mkazi Mahakama ya Wilaya ya Uvinza, Misana Majura amesema kuwa Mahakama imejiriridhisha pasipo shaka na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka na hatimae kumtia hatiani mtuhumiwa kwa kosa hili.
Mshitakiwa amehukumiwa kifungo hicho ili iwe fundisho kwa wahalifu wanaojihusisha na vitendo vya uwindaji haramu ambavyo vinapelekea uharibifu wa rasilimali za taifa ikiwemo Wanyama pori.