Mahakama ya Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro imemhukumu Omari Bokoi, mshtakiwa katika shauri namba 11/2018 la uhujumu uchumi na makosa ya kupanga kulipa faini ya Milioni 333 au kwenda jela miaka 20 baada ya kumkuta na hatia ya kupatikana na vipande vya nyama ya Twiga .
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Same Helen Hoza ambapo pia mahakama imewaachia huru washtakiwa wengine wawili katika shauri hilo baada ya kukosekana kwa ushahidi wa kutosheleza kuwatia hatiani.
Bokoi amehukumiwa baada ya kupatikana Nyara za Serikali kinyume cha sheria ya uhifadhi wa wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 inayosomwa sambamba na kifungu cha 14 cha jedwali namba 1 na kifungu namba 57 kifungu kidogo cha kwanza na kifunga cha 60 kifungu kidogo cha pili cha sheria ya uhujumu uchumi na makosa ya kupanga.
Akisoma maelezo ya kosa kwa watuhumiwa hao, Hakimu Hoza ameeleza kuwa mnamo Oktoba 15 mwaka 2018, katika eneo la Muheza jirani na Hifadhi ya taifa ya Mkomazo Wilayani Same, washtakiwa hao walikutwa na vipande vya nyama ya Twiga .
Katika shauri hilo Mwendesha mashtaka wa shirika la Hifadhi za taifa (TANAPA) Samuel Magoka kwa niaba ya Jamhuri aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa yeyote mwenye nia ya kufanya vitendo vya ujangili kwa Nyara za Taifa.
Aliieleza Mahakama kuwa wanyama jamii ya Twiga wameendelea kutoweka na serikali iimekuwa ikitumia gharama kubwa katika kuwalinda, pia ni nembo ya taifa na ni kivutio cha watalii katika kuiingizia serikali fedha za kigeni.
Mshtakiwa baada ya hukumu kutolewa ameshindwa kulipa faini hivyo ataenda kutumikia miaka 20 jela.