Beki wa zamani wa klabu ya Young Africans, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ amemshauri kocha mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Sven Vandenbroeck, kuhusu safu ya ulinzi ya klabu hiyo.

Malima ametoa ushauri kwa kocha Sven, huku akiamini safu ya ulinzi ya Simba SC ina mapungufu hususana wanapocheza kwa pamoja wakongwe Pascal Wawa na Joash Onyango.

Amesema pamoja na kuhofia mchezo wa mkondo wa pili endapo wataendelea kuwatuamia wachezaji hao wa kigeni, pia kuna hatari ya kufanya vibaya kwenye michezo ya Ligi Kuu na kombe la Shirikisho (ASFC).

“Kocha Sven endapo ataendelea kuwatumia mabeki Joash Onyango na Pascal Wawa kama alivyofanya kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa mjini Harare juma lililopita, kuna hatari matokeo yakaendelea kuwa mabaya wa Simba SC.”

“Safu ya ulinzi ya Simba ina upungufu mkubwa na sio katika mchezo huo tu dhidi ya Platinum, lakini hata michezo mingine wanafanya sana makosa,”

“Nafikiri ni muda wa kurekebisha hilo haraka. Sio kwamba ni mabeki wabaya, lakini nafikiri wale wawili wote ni wazee, hivyo hawana kasi ya kukabiliana na washambuliaji wenye kasi kama wakiendelea kucheza pamoja.

“Kinachotakiwa pale nyuma asimame mtu mzima mmoja na kisha waweke beki mwingine kijana, mambo yatakuwa vizuri kwani naamini watacheza kwa maelewano na watasikilizana kuliko wanavyocheza sasa kwa pamoja Wawa na Onyango.” Amesema Jembe Ulaya.

Simba SC itakua mwenyeji kwenye mchezo wa mkondo wa pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya FC Platnum ya Zimbabwe Januari 06, Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es salaam, huku ikikumbuka kupoteza mchezo uliopita kwa kufungwa bao moja kwa sifuri.

Trump asaini Bilioni 900 za misaada ya COVID-19
Makampuni ya simu yapewa miezi mitatu tatizo la 'bando'