Mchambuzi wa Michezo nchini Tanzania Jemedari Said Kazumari amewakosoa baadhi ya wadau wa soka wanaopinga mfumo wa upangaji kikosi wa Kocha Mkuu wa Simba SC.
Kocha Franco Pablo Martin alifanya mabadiliko kwenye kikosi chake jana Jumatatu (Januari 17) dhidi ya Mbeya City, na mwisho wa dakika 90 mambo yalimuendea kombo kwa kufungwa bao 1-0.
Jemedari amesema: “Wale wanamkosoa Kocha wa Simba SC kufanya Mabadiliko (ROTATIONS) kwenye kikosi chake mara kwa mara ikiwemo jana walipopoteza na Mbeya City, wanapata wapi ujasiri huo KIUFUNDI kutokana na Ratiba hiyo hapo?”
“Hapo ndani yake kuna siku za mazoezi (maandalizi) kutoka mechi moja kwenda nyingine, kuna siku za safari ambazo kati ya 1-2 kulingana na umbali, ukiweka akilini siku za safari hakuna mazoezi.”
“Hujapata minor injuries & illness kwa players wako. Watu wakumbuke wachezaji ni binadamu na wanahitaji mapumziko kila baada ya kazi ngumu ili ku-recover pia. Bahati mbaya mpira kila mmoja wetu anaujua kuliko wajuzi wenyewe”
Baada ya mchezo wa jana Jumatatu (Januari 17), Simba SC itacheza dhidi ya Mtibwa Sugar Jumamosi (Januari 22) Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, kisha itacheza dhidi ya Kagera Sugar Jumatano (Januari 26).