Mchambuzi wa Soka la Bongo Jemedari Said Kazumari ni kama amezipiga Kijembe Klabu za Young Africans na Azam FC, baada ya Simba SC kuibuka na ushindi wa 3-1 ugenini.

Young Africans ililazimishwa matokeo ya sare ya 1-1 nyumbani Dar es salaam dhidi ya Mabingwa wa Sudan Al Hilal kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Azam FC ikipoteza mchezo wake wa Kombe la Shirikisho ugenini, dhidi ya Al-Akhdar ya Libya kwa mabao 3-0.

Akiwa katika Kipindi cha SPORTS HQ cha EFM mapema leo Jumatatu (Oktoba 10) asubuhi, Jemedari amesema ushindi wa Simba SC umoenyesha ukomavu na utayari wa wachezaji wa klabu hiyo linapokuja suala la kushindana kimataifa, tofauti na wawakilishi wengine wa Tanzania, ambao walikua viwanjani mwishoni mwa juma lililopita.

Amesema Simba SC imedhihirisha ukubwa wake kwenye Michuano ya Kimataifa na kuifanya Primeiro De Agosto kuonekana timu ya kawaida, kitu ambacho sio kweli.

“Tunaposema kuna Simba halafu kuna vilabu vingine muwe mnaelewa. Leo D’Agosto wanaonekana wa kawaida kwa kuwa wamekutana na moja ya klabu Bora Afrika na wamezidiwa, sio kila timu ingeshinda hapa.” amesema Jemedari Said

Simba SC itacheza mchezo wa Mkondo wa Pili dhidi ya Primeiro De Agosto Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam Jumapili (Oktoba 16), huku ikitakiwa kusaka ushindi wa aina yoyote ama sare, kujihakikishia nafasi ya kutinga Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Young Africans itacheza ugenini Omdurman-Sudan Jumamosi (Oktoba 15) dhidi ya Mabingwa wa Sudan Al Hilal, huku ikitakiwa kusaka ushindi wa aina yoyote ama sare kuanzia 2-2, ili kujihakikishia nafasi ya kutinga Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Kwa upande wa Azam FC wao watacheza nyumbani Azam Complex-Chamazi jijini Dar es salaam Jumapili (Oktoba 16) dhidi ya Al-Akhdar, huku wakilazimika kusaka ushindi wa 4-0, ambao utawavusha hadi hatua inayofuata katika Michuano ya Kombe la Shirikisho.

Edo Kumwembe: Nasreddine Nabi alijinyonga mwenyewe
Kocha Young Africans aahidi ushindi Sudan