Mshambuliaji wa Soka la Bongo Jemedari Said Kazumari ameendelea kulivalia njuga sakata la Msemaji wa Young Africans Haji Manara, kufuatia kupishana kauli na Rais wa Shirikisho la soka Tanzania ‘TFF’ Wallace Karia.
Manara ameonekana katika video fupi akizungumza kwa ukali dhidi ya Karia wakati wa mchezo wa Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ uliopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha Jumamosi (Julai 02), kati ya Young Africans na Coastal Union.
Jemedari ambaye alikua wa kwanza kurusha video za Manara alipokwaruzana na Karia, amedai kupokea vitisho vya kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kumchafua Msemaji wa Young Africans kwa madai ya kuandika uongo.
“Licha ya Maneno ya Vitisho na Ukosoaji usiokua na mashiko juu ya Habari niliyoiweka wazi Kuhusu Msemaji Dhidi ya Rais wa TFF, Sheria ndio itaamua kwa asilimia zote nani mwenye haki kwenye hili”
“Sipo katika vita ya kumshusha mtu au kuchafua Brand ya mtu kwenye hili, kamati za maadili zipo na zitaendesha jambo hili kimaadili, mimi nilitoa habari kama tunavyotoaga habari zingine kitu ambacho ndio kazi yangu kila siku”
“Ushahidi ambao Msemaji jana kasema ukitoa atajiuzulu, upo na watu wengi wapo wa kuzungumza, watu wana clip nzuri zaidi ya ile niliyoweka ambayo sauti zinasikika, ila kimaadili na sheria wamezihifadhi, zipo na zitatoka kisheria kama ushahidi wa kesi hii ya kimaadili ambayo TFF Wameitoa jana taarifa.” Amesema Jemedari Said