Mchambuzi wa Michezo nchini Tanzania Jemedari Said Kazumari anaamini baadhi ya waamuzi wa soka wanaochezesha Ligi Kuu Tanzania Bara wanafanya makosa kwa makusudi ili kuwaridhisha wanaowakusudia.
Jemedari amesema waamuzi wa Tanzania wanafahamu misingi na taratibu za kuchezesha Soka na ndio maana wanapoteuliwa kuchezesha michezo ya Kimataifa hawafanyi makosa ya kupuuzi.
Amesema amewafuatilia baadhi ya waamuzi ambao huteuliwa kuchezesha michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika na kubaini wamekua wakitenda haki kwa kufuata sheria 17 za Soka, lakini hao hao hupindisha sheria hizo wanapokua kwenye majukumu ya Ligi ya Tanzania Bara.
“Waamuzi wa Tanzania wanafanya makusudi kabisa, binafsi ninaamini hilo, nimewafutilia kwa muda mrefu na nimebaini kuna makusudi wanayafanya ili kuwaridhisha baadhi ya watu.”
“Hawa waamuzi mbona wanapokua kwenye majukumu ya Kimataifa hawalalamikiwi? Kwa nini wanapochezesha katika Ligi ya Tanzania Bara hawaishi kulalamikiwa? Binafsi nafahamu kuna makusudi yanafanywa hapa.”
“Ni aibu kwa Soka la nchi yetu, tuna watu ambao wanajua kabisa wanapaswa kufanya nini, lakini wanafanya ujinga kwa kusudi la kulifurahisha kundi la watu fulani.” amesema Jemedari Said
Waamuzi wa Soka la Bongo wamekua kwenye lawama kila kukicha kufutia makosa ya uchezeshaji, kitu ambacho kinaleta mgongano wa mawazo, ambapo baadhi ya wadau wanaamini wanafanya hivyo kwa makosa ya kibinaadamu, lakini wengine kama Jemedari Said hawaamini hivyo.