Meneja wa mlinda mlango wa Young Africans Metacha Mnata amesema mchezaji wake alifanya kitendo cha ‘kishamba’ kwa kuzozana na mashabiki na kuwaonesha alama za matusi.
Jemedari Said, meneja wa Mlinda Mlango huyo ambaye jana alikubali kufungwa mabao mawili, licha ya timu yake Young Africans kuibuka na ushindi wa mabao matatu, amemlaumu Metacha kupitia kipindi cha michezo cha Radio E FM leo asubuhi.
Jemedari amesema makosa aliyofanya Metacha uwanjani ni ya kawaida, yanarekebishika, lakini kuzozana na mashabiki haikuwa sawa hata kidogo.
“Nilimuambia umekosea mdogo wangu…” amesema Jemedari.
Tayari Uongozi wa Young Africans umetangaza kumsimamisha kwa muda Metacha Mnata kwa kosa la utovu wa nidhamu aliouonesha jana baada ya mchezo dhidi ya Ruvu Shooting.
Metacha alifikia hatua ya kuonesha utovu wa nidhamu baada ya kuchukizwa na maneno makali yaliyotolewa dhidi yake na baadhi ya mashabiki wa Young Africans, ambao walidai alifungisha kwa makusudi bao la pili kwenye mchezo huo.
Ushindi wa mabao matatu kwa mawili dhidi ya Ruvu Shooting, unaiwezesha Young Africans kufikisha alama 64, ambazo zinaendelea kuiweka nafasi ya pili klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.