Mdau wa Soka nchini Tanzania Jemedari Said ameonesha kukerwa na kejeli zinazotolewa na baadhi ya Mashabiki dhidi ya ushindi wa Simba SC Kimataifa.

Simba SC ilivuna ushindi wa 3-1 dhidi ya Primero de Agosto Jumapili (Oktoba 09) ugenini Luanda-Angola, na kujiweka katika mazingira mazuri kuelekea mchezo wa Mkondo wa Pili, ambao utapigwa Jumapili (Oktoba 16) Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Ushindi huo wa Simba dhidi ya Primero de Agosto ulizua kejeli kwa baadhi ya Mashabiki ambao waliandika katika Mitandao ya Kijamii wakisisitiza timu hiyo ya Angola ni dhaifu, kwani iliwahi kupoteza dhidi ya Namungo FC kwa kufungwa 6-2 katika michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu miwili iliyopita.

Kejeli hizo zimemuibua Jemedari na kuwajibu Mashabiki hao kupitia kurasa zake za Mitandao ya Kijamii kwa kuandika: SIMBA IPEWE HESHIMA YAKE.

Tunaposema kuna Simba halafu kuna vilabu vingine muwe mnaelewa. Leo D’Agosto wanaonekana wa kawaida kwakuwa wamekutana na moja ya klabu Bora Afrika na wamezidiwa, sio kila timu ingeshinda hapa.

Nimeona watu wanaleta ushahidi wa mechi dhidi ya Namungo ambayo wachezaji 8 bora wa Premeiro D’Agosto walizuiwa kucheza kwa “Mizengwe” ya UVIKO 19.

Hata baada ya kufungwa 6-2 pale Chamazi ambako zilichezwa mechi zote 2, lakini Namungo kwenye Group stage HAWAKUWEZA kufunga hata bao 1, kitu kilichoonyesha bila zengwe la UVIKO 19 pengine wasingekuwepo kwenye makundi.

SIMBA SC ipewe heshima yake, timu zetu zoote zinaweka malengo ya kucheza Makundi, Simba SC peke yao ambao malengo yao ni NUSU FAINALI.

Ukiona wanavyocheza wanakuonyesha hawapangi malengo kwa bahati mbaya. Yes, wana mapungufu kulinganisha na WAKUBWA wenzao wa Africa, lakini nyie wengine HAMJIWEZI kwenye hizi anga zao tuweni wakweli tu.

Mara nyingine ukiona Elimu mnayotoa inaingia vichwani mwa watu kidoo kidogo unafarijika.
BIN KAZUMARI (Voice of the voiceless)

Young Africans yawajibu wachambuzi, kusafiri kesho
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Octoba 14, 2022