Mchambuzi wa Michezo kupitia kituo cha Radio cha EFM, Jemedari Said ameushukia Uongozi wa klabu ya Young Africans kwa kusema unapaswa kupokea lawama zote za klabu hiyo kuondolewa mapema kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Young Africans imetupwa nje ya michuano hiyo, baada ya kufungwa na Rivers United ya Nigeria jumla ya mabao 2-0.
Jana Jumapili (Septamba 19) Young Africans walipoteza kwa kufungwa bao 1-0 ugenini kama ilivyokua nyumbani jijini Dar es salaam (Septemba 12) wapopoteza kwa idadi hiyo Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Jemedari amesema: “Sitapindisha. Makosa makubwa Yanga yapo kwa viongozi. Walipaswa kujua kwamba wana jukumu la kuwakilisha nchi kimataifa. “
“Tuliona kipindi cha usajili, mmoja wa viongozi wanaofanya usajili Yanga alipokwenda DR Congo akaanza mizunguko mingi na akisindikizwa na magari ya kijeshi kwa mbwebwe…”
“Unaenda kuwatafuta wachezaji ili kuwatumia kimataifa lakini unashindwa kuwatumia..hapo huwezi kumrushia lawama mwalimu (Kocha).”
Kuondolewa kwa Young Africans kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, kumeipunguzia Tanzania nafasi ya timu moja kwenye michuano ya barani humo, baada ya CAF kuiweka Tanzania kwenye orodha ya nchi zilizoingia timu nne msimu huu 2021/22.
Kwa sasa Tanzania imebakiwa na timu tatu ambazo ni Simba SC itakayoanzia hatua ya kwanza ya Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, huku Azam FC na Biashara United zikitinga hatua ya kwanza wa michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, baada ya kushinda michezo yao ya hatua ya awali.