Kamishna Jenerali wa Magereza nchini Tanzania, Phaustine Kasike amefurahishwa na ushirikiano wa Serikali ya Mkoa wa Kagera chini ya Mkuu wa Mkoa huo, Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti na Jeshi la Magereza kwa namna wanavyoshirikiana kutatua changamoto mbalimbali za Jeshi hilo katika kuweka mazingira bora ya utendaji kazi.

Jenerali Kasike amempongeza mkuu wa mkoa huo pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kwa kudumisha ulinzi na usalama hasa kwa kipindi hiki ambacho kwasasa mkoa wa Kagera umetulia kwa matukio mbalimbali makubwa ya utekaji barabarani.

Amesema kuwa yupo Mkoani Kagera kwa ziara ya kikazi hasa kufuatilia maelekezo mahususi yaliyotolewa kwa Jeshi hilo ya kuhakikisha Jeshi la Magereza linazalisha chakula cha kutosha kuwalisha wafungwa.

“Sisi Jeshi la Magereza tumeweka mkakati maalumu wa kuzalisha chakula cha kutosha kulisha Magereza yote nchini na katika mkakati huo tulibainisha Magereza kumi nchi nzima ambapo na Gereza la Kitengure la hapa mkoani Kagera lipo kati ya hayo kumi kwani Gereza hilo linazalisha chakula kwa misimu miwili ya vuli na masika.”amesema Jenerali Kasike.

Aidha, amesema kuwa katika kuboresha makazi ya maafisa wa Jeshi la Magereza, wanampango mkakati wa Kila Gereza kuzalisha tofali hasa zile za kuchoma ili kujenga makazi mapya ya maafisa na kukarabati miundombinu ambayo tayari imechoka.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa huo, Jenerali Marco Gaguti amemshukuru Kamishna Jenerali Kasike kwa kuamua kufanya ziara Mkoani Kagera kujionea changamoto mbalimbali hasa kwa upande wa chakula cha wafungwa na makazi ya maafisa wa Jeshi la Magereza.

Wakulima wa Kilimo cha Umwagiliaji wapigwa msasa
Ole Sendeka atoa maagizo mazito