Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Uganda Jenerali Katumba Wamala ametoa ujumbe mapema leo akimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumuokoa na kubakia hai baada ya shambulio lililomlenga mapema jana Jumanne katika eneo la Kiasasi jijini Kampala.

Katika ujumbe alioutoa kwenye video fupi iliyorekodiwa kutoka Hospitali ya Medipal, Jenerali Katumba ambaye aliwahi kuwa waziri wa ulinzi wa Uganda amesema: ‘’Mungu amenipa fursa nyingine. Nitakuwa vyema tena msiwe na wasiwasi, sina majeraha mabaya, ni mikono tu, lakini nitakuwa sawa.”

Katumba amesema yuko pamoja na madaktari wanaofanya kila liwezekanalo kuokoa maisha yake.

Binti yake Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Uganda, Brenda Nantongo, na dereva wake waliuawa katika shambulio lililofanywa na watu wanne ambao walikuwa kwenye pikipiki.

Amesema hajui sababu ya shambulio hilo na kwamba hapakuwapo sababu ya kumaliza maisha ya watu wasio na hatia.

Picha zilizoenea katika mitandao ya kijamii zimeonyesha matundu ya risasi katika dirisha la gari huku vipande vya vioo vikiwa vimetapakaa chini katika eneo la tukio.

Jaribio la mauaji dhidi ya Katumba Wamala limetokea katika eneo hilo hilo palipojiri mauaji ya afisa wa polisi mwaka 2017 aliyejulikana kwa jina la Felix Kaweesa.

Afisa huyo wa polisi aliuliwa na watu waliokuwa na silaha waliokuwa wamepanda pikipiki.

Yanga SC yamkana Ibrahim Ajibu
Nabi: Yanga itakua tishio Afrika