Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo ameupongeza uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala kwa kusimamia vizuri ujenzi wa Jengo jipya la kisasa la Mama na Mtoto litakaloanza kutoa huduma hivi karibuni.

Akizungumza wakati alipofanya ziara katika hospitali hiyo, Chongolo amesema kuwa jengo hilo ambalo limejengwa kwa fedha za Serikali litakuwa mahususi kwa wananchi wa maeneo yote yaliyopo ndani na nje ya Manispaa hiyo kwa kuwa litatoa huduma nyingi ambazo awali hazikuwepo.

Chongolo amesema kukamilika kwa hatua za mwisho kwa jengo hilo kutatoa fursa ya huduma za upimaji kwa kutumia CT-SCAN, ‘Private Room’, kitu ambacho awali hakikuwepo Hospitalini hapo na kwamba wananchi watapata huduma hiyo kwa ufanisi mkubwa.

“ Nimefurahishwa na kazi nzuri ambayo imefanyika, ninawapongeza kwa namna ambavyo mnashirikiana kuhakikisha kwamba matumizi ya jengo hili yana anza rasmi, nitarudi tena kujiridhisha katika maandalizi ya jumla kabla ya kuanza kulitumia hili jengo jipya la huduma ya mama na Mtoto” amesema Chongolo.

“Nategemea matokeo kwa haraka ili wale ambao wanapata huduma ya Afya katika Hospitali yetu ya Rufaa ya Mkoa, Mwananyamala waanze kupata huduma iliyo bora, Serikali ya Rais Dk. Magufuli inafanya kazi kubwa, imetoa fedha nyingi kiasi cha Bilioni 2.2 kwa ajili ya Hospitali hii kuboresha huduma inahitaji pia kuona matokeo ya haraka”ameongeza Chongolo.

Jengo hilo linatarajiwa kuwa na vitanda, 78 kwa ajili ya watu wazima, Watoto wachanga, Wodi ya Mama na Mtoto, Mama wajawazito, huduma za kujifungulia, sambamba na wale wanaohitaji huduma maalum.

Koeman aukubali muziki wa Barcelona
Serikali yatenga Bil. 4 kuimarisha miundombinu Jangwani