Helikopta za Jeshi la Israel zimeshambulia maeneo ya kusini mwa Syria, Ijumaa, Julai 24, 2020 kwa madai kuwa wanalipa kisasi kwakuwa ilishambuliwa kwa makombora kutoka ndani ya Syria.
Hatua hiyo imeongeza uhasama na taharuki kati ya nchi hizo mbili. Mashambulizi ya Israel yameripotiwa saa chache baada ya Jenerali wa ngazi za juu wa Marekani, Mark Milley kutembelea nchi hiyo.
Ilielezwa kuwa Jenerali Milley alifanya mazungumzo kuhusu jinsi ya kuvidhibiti vikosi vya Syria na nchi zinazoiunga mkono.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AFP, awali, Israel ilidai kuwa Syria ilirusha vilipuzi kuelekea eneo la Golan, eneo ambalo vikosi vya Waisrael vilikuwa vinalikalia tangu mwaka 1967. Ilidai kuwa vilipuzi hivyo viliwajeruhi watu kadhaa, kuharibu gari na nyumba za raia.
“Maeneo mbalimbali yalishambuliwa ikiwa ni pamoja na maeneo yenye mfumo wa kiintelijensia katika ngome ya SAF,” taarifa ya Jeshi la Israel ilieleza.
Shirika la Habari la Syria (NASA), liliripoti kuwa makombora ya Israel yalipiga katika maeneo matatu, yalijeruhi watu wawili na kusababisha moto mkubwa kuwaka msituni.