Jeshi la Marekani limekiri Ndege yake kutunguliwa na jeshi la Iran ilipokuwa kwenye anga ya kimataifa kwenye eneo la mpaka kati ya ghuba ya Oman na Uajemi.

Awali vikosi vya jeshi vya Iran vilidai kuwa vimeshambulia ndege ya kijasusi isiyo na rubani ambayo ilikuwa katika anga la Iran.

Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti tukio hilo dhidi ya ndege isiyokuwa na rubani waliyoiita RQ-4 Global Hawk, kusini mwa jimbo la Hormozgan.

Aidha, jeshi la Marekani awali halikuthibitisha kama ndege yake imeangushwa, huku msemaji akikana taarifa kuwa ndege ya Marekani ilikuwa kwenye anga la Iran.

Tukio hilo limetokea siku chache baada ya wizara ya ulinzi ya Marekani kusema kuwa watapeleka vikosi vya wanajeshi 1,000 katika eneo la Mashariki ya Kati baada ya kutokea mvutano kati ya Marekani na Iran.

Mzozo huo ulishika kasi siku ya Jumatatu wakati Iran iliposema kuwa itazidisha kiwango cha urutubishaji wa madini ya Uranium kinyume cha makubaliano na mataifa yenye nguvu duniani yaliyofanyika mwaka 2015.

Hata hivyo, mgogoro kati ya nchi hizo mbili ulianza mwaka jana mara baada ya rais wa Marekani, Donald Trump kutangaza kujitoa katika mkataba wa kimataifa wa mwaka 2015 uliolenga kumaliza mpango wa nyuklia nchini Iran.

 

Njiti za masikio zatajwa chanzo cha ukiziwi
Bibi harusi mtarajiwa afa ajalini