Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani kimetoa kofia ngumu 300 na makoti ya kuakisi mwanga 250 katika halmashauri ya mji wa Makambako Mkoa wa Njombe, kwa madereva bodaboda na bajaji ikiwa ni muendelezo wa kampeni ya Safiri Salama inayotolewa na jeshi hilo ambapo kupitia kampeni hiyo wanatoa elimu ya usalama barabarani kwa madereva wa vyombo vya aina zote.

Akizungumza na Kituo cha Habari cha Dar24, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini ACP Wilbrod Mutafungwa amesema kuwa madereva 500 wamepata elimu ya msasa kwa wiki moja kutoka kwa wataalamu wa kikosi cha usalama barabarani wakishirikiana na Chuo cha Wide Institute cha mkoani hapo, Ofisi ya Mkoa usalama barabarani na LATRA.

Aidha Kamanda Mutafungwa amewaasa askari wote wa usalama barabarani kupitia madawati yote vituoni wajikite kwenye suala zima la utoaji elimu ya usalama barabarani ili kusaidia kupunguza zaidi ajali za barabarani.

“Kwahiyo tukiendelea kutoa elimu zaidi itasaidia kushusha kabisa viwango vya ajali barabarani lakini pia itatengeneza mazingira ya sisi kuwa karibu na wadau wetu madereva bajaji, bodaboda na madereva wote,” amesema Kamanda Mutafungwa.

Mafunzo waliyoyapata ni pamoja na utii wa sheria za usalama barabarani, alama za barabarani na jinsi ya kuepukana na hali hatarashi za barabarani kama vile umuhimu wa kuvaa kofia ngumu, makosa ya mwendokasi, ku ‘ovateki’ sehemu isiyoruhusiwa na mengineyo.

Hata hivyo, Kamanda Mutafungwa amesema kuwa mpango wa Safiri Salama ni mpango ambao unawagusa hata wanachi wa kawaida, wasafiri na watoto wa mashuleni na unatekelezwa nchi nzima.

Meya aagiza kusitishwa ununuzi wa bastola ya Mkurugenzi
Mahakama ya Mali yamtangaza Rais wa mpito