Jeshi la polisi nchini limepiga marufuku maandamano ya wagombea urais wa vyama mbalimbali vya siasa wakati wakichukua fomu, kutafuta wadhamini au kurudisha fomu hizo katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, D/IGP Abdulahman Kanini ametoa tamko hilo la jeshi leo jijini Dar es Salaam, katika mkutano na waandishi wa habari.

Akitoa sababu za kuchukua uamuzi huo, D/IGP Kanini alisema kuwa wamchukua uamuzi huo kutokana na sababu za kiusalama kufuatia maandamano hayo makubwa yaliyoshuhudiwa hivi karibuni wakati wa uchukuaji fomu wa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa na Dk. John Magufuli.

“Sababu kuu ambazo zinasababisha tusitishe maandamano haya ni za kiusalama. Ni baada ya tathmini ambayo tulifanya, kufuatia zoezi la kuchukua fomu la chama kile cha awali na chama kile kingine,”alisema.

Alisema jeshi hilo lilipokea malalamiko kutoka kwa wananchi wakidai kushindwa kufanya shughuli zao za kiuchumi na kijamii na kupata usumbufu kutokana na maandamano hayo.

“Kila mtu ana haki ya kufanya hayo. Lakini inabidi wafanye hivyo kwa kufuata sheria. Maandamano yana taratibu zake, na sidhani kama utaratibu huo ulifuatwa,” aliongeza.

Wiki iliyopita, shughuli mbalimbali zilisimama kwa muda jijini Dar es Salaam kupisha maandamano ya maelfu ya wafuasi wa Ukawa walimsindikiza mgombewa wa Chadema kupitia umoja huo, Edward Lowassa alipoenda kuchukua fomu katika ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

 

 

Kumbe Mourinho Alimtusi Eva Carneiro (Video)
Wenyeviti Wengine Wa CCM Watimkia Chadema