Jeshi la Polisi Mkoani Pwani limewaua watu wanne wanaodhaniwa kuwa wahalifu wanaojihusisha na mauaji yanayoendelea Wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Operesheni Maalumu wa Jeshi hilo, Naibu Kamishna wa Polisi, Liberatus Sabas ambapo amesema kuwa tukio hilo limetokea saa tatu usiku Juni 29 mwaka huu.
Amesema kuwa wakati Polisi wakiwa katika doria katika barabara ya Pagae kuelekea Nyambunda walikutana na kikundi cha watu takribani sita hivyo mara baada ya kuiona gari ya Polisi walikimbilia vichakani huku wakianza kuwarushia risasi Polisi.
“Katika tukio hilo tumefanikiwa kupata silaha mbili aina ya SMG na Magazine mbili pamoja na risasi 17 zilizokuwa zikitumiwa na wahalifu hao na hii ni dalili ya kuwa tunaendelea vizuri na operesheni yetu ambayo inashirikisha na vyombo vingine vya usalama katika wilaya hizi tatu za Kibiti, Mkuranga na Rufiji,”amesema Sabas
Hata hivyo, Sabas ametoa wito kwa wahalifu kuacha mara moja tabia hiyo kwani vyombo vya usalama vinafanya operesheni ya kutokomeza uhalifu huo katika maeneo hayo.