Jeshi la polisi Tanzania limetoa ufafanuzi juu ya tukio la kujinyonga hadi kuzikwa kwa askari mmojawapo kati ya waliohusika katika mauaji ya mfanyabiashara wa madini mkoani mtwara.
Katika barua yake kwa vyombo vya habari Msemaji wa jeshi la polisi Tanzania, David Misime, ametoa maelezo ya namna tukio la kukamatwa kwa Grayson Mehembe na wenzake ikiwa ni pamoja na maelezo aliyoyatoa kwa Jeshi la Polisi ya jinsi walivyomuua Mfanyabiashara huyo.
Barua hiyo inasema kuwa baada ya kugundulika kujinyonga katika mahabusu ya pekeyake, taratibu zote za kipolisi zilifuatwa hadi kuzikwa kwake.
Hata hivyo barua hiyo inasema kuwa katika taratibu za Jeshi la Polisi, Askari anayejinyonga hazikwi kwa taratibu za kijeshi kwa sababu anahesabika hakufariki kishujaa hivyo mwili wake hukabidhiwa kwa familia yake na kuzikwa kifamilia.