Jeshi la Polisi, limetajwa kuwa ni miongoni mwa taasisi za utoaji haki nchini ambayo inanyooshewa vidole na kulalamikiwa na wananchi juu ya rushwa kutokana na upindishaji wa haki na kuchepusha sheria.
Hayo yamebainishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Jumanne Januari 31, 2023 jijini Dodoma na kuongeza kuwa ukiongea na watu 70 kati ya 100 watakuwa wakililalamikia utendaji wa jeshi hilo.
Rais Samia ambaye alikuwa akiongea wakati wa hafla ya uzinduzi tume ya kuangalia jinsi ya kuboresha taasisi za haki jinai nchini amesema, Tume hiyo imepewa miezi minne kuanzia kesho (Februari 1- Mei, 2023), kukamilisha na kukabidhi ripoti hiyo.
Aidha, amezitaja taasisi zitakazochunguzwa kuwa ni jeshi la Polisi, Mahakama, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya ili kufahamu mapungufu yaliyopo, mifumo ya ajira na mafunzo, matumizi ya tehama na teknolojia, utendaji kazi, upandishaji vyeo na wananchi jinsi wanavyozitazama taasisi hizo.