Wanajeshi wa Rwanda waliotumwa nchini Msumbiji mwezi uliopita kulisaidia jeshi la nchi hiyo kupambana na wapiganaji wanaojiita ‘Al Shabaab’, waliokuwa wameshikilia jiji la bandari la Mocimboa da Praia, wamesema wamefanikiwa kulirejesha eneo hilo lililokuwa ngome ya adui.

Wapiganaji hao, ingawa wanajiita Al-Shabaab hawana uhusiano na kundi la Al-Shabaab la Somalia, lakini hutumia jina hilo kumaanisha ‘vijana’ kwa lugha ya kiarabu.

“Jiji la Bandari la Mocimboa da Praia, ambalo ni ngome ya wapiganaji hao kwa kipindi cha miaka miwili limerejeshwa kutokana na kazi iliyofanywa na wanajeshi wa Rwanda kwa kushirikiana na wanajeshi wa Msumbiji,” taarifa ya Jeshi la Rwanda imeeleza kupitia ukurasa wao wa Twitter.

Ingawa kundi la waasi bado halijatoa taarifa yoyote, hatua hii inaonesha ushindi mkubwa kwa Serikali ya Msumbiji katika vita hiyo iliyokuwa inaendelea upande wa Kaskazini mwa nchi hiyo.

Mwezi uliopita, Rwanda ilituma wanajeshi 1,000 kuongeza nguvu kwa jeshi la Msumbiji dhidi ya wapiganaji hao walianza operesheni za mapigano mwaka 2017.

Zaidi ya watu 3,000 wameripotiwa kuuawa na 820,000 hawana makazi tangu hali ya mapigano ilipozuka.

Waziri wa kilimo amtumbua Meneja ununuzi wa mbolea.
Mwandishi wa habari auawa DRC.