Jeshi la Uganda limezungumzia hatua iliyochukuliwa na vyombo vya usalama kuwaondoa kwa nguvu wabunge waliotimuliwa bungeni na Spika, Rebbeka Kagada, Jumatano wiki hii.
Akizungumzia uamuzi huo, Jenerali Elly Tumwine alisema kuwa uamuzi huo ulikuwa sahihi kwani wabunge hao walivunja sheria na kwenda kinyume na kanuni zinazowalinda ndani ya bunge hilo kwa kufanya vurugu na kupigana.
Wabunge 25 wa upinzani walisimamishwa na Spika wa Bunge hilo baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika katika vurugu iliyosababisha vikao vya bunge kusimamishwa kwa muda. Vurugu hizo ziliibuka wakati mjadala wa kuondoa ukomo wa umri wa kugombea urais ulipowasilishwa bungeni.
Vurugu hizo zilihusisha mapigano ya ngumi, kukabana na kurushiana viti kati ya wabunge wa kambi ya upinzani na wabunge wa chama tawala kinachomuunga mkono Rais Yoweri Museveni pamoja na mawaziri wake.
Mbali na vurugu hizo ndani ya Bunge, kiongozi wa chama cha upinzani ambaye ni mpinzani mkuu wa Rais Museveni, Kizza Besigye alishikiliwa na jeshi la polisi baada ya kutaka kufanya maandamano ya kupinga muswada huo.
Kwa mujibu wa ibara ya 102 (b) ya Katiba ya nchi hiyo, ukomo wa umri wa kugombea urais ni miaka 75 tu. Hivyo, kifungu hicho kingewemzuia Rais Museveni mwenye miaka 73 kugombea urais katika awamu nyingine.