Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Nchini, liko katika mkakati wa kuingia ushirikiano na Serikali ya Kuwait katika shughuli zake za kukabiliana na majanga ya moto ikiwa ni juhudi zake katika kuyafikia maeneo mengi nchini.

Hayo yamejiri baada ya Balozi wa Kuwait Nchini, Jasem Al-Najem alipotembelea Makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji jijini Dar es salaam, ambapo ameeleza kuwa serikali ya Kuwait ipo tayari kubadilishana mafunzo na kutoa msaada wa vifaa kwa Jeshi hilo.

“Ni vema tukatengeneza mpango ambao wataalam wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kutoka nchini Tanzania wataweza kubadilishana uzoefu na wataalamu kutoka nchini Kuwait kwa ajili ya kujifunza mbinu mbalimbali za kukabiliana na majanga pindi yanapotokea, ’’ Alisema Balozi huyo.

Naye, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye alimshukuru kwa kumtembelea na kusema kuwa ujio wa balozi huyo, umefungua ukurasa mpya kwa upande wa misaada na mafunzo kwa Askari wa Jeshi hilo, kwani watapata fursa ya kubadilishana uzoefu na kuongeza tija kwa Jeshi lake.

“Tutapata nafasi ya kubadilishana uzoefu na kupata mafunzo kutoka Nchi ya Kuwait na kuongeza ufanisi katika majukumu yetu ya kila siku, lengo ikiwa ni kukabiliana na majanga mbalimbali yakiwemo ya moto,’’ alisema Kamishna Jenerali.

Katika kikao hicho Balozi wa Kuwait, Nasem Al-Najem alipokea taarifa ya changamoto zinazolikabili jeshi hilo ikiwemo uhaba wa vitendea kazi huku akiahidi kuzifanyia kazi na akisisitiza mchakato wa kusaini makubaliano ya hiari ukamilike kwani utakuwa msaada wa kutekeleza kwa haraka program za mafunzo ya muda mfupi.

Putin awatimua wamarekani nchini Urusi
Magazeti ya Tanzania leo Agosti 1, 2017