Jeshi la Sudan limesema halitakubali kuiona Serikali ya nchi hiyo ikianguka kutokana na maandamano yanayoendelea yanayotaka Rais Omar al-Bashir ajiuzulu.
Mkuu wa Majeshi, Jenerali Kamal Abdul Maarouf amesema kupitia taarifa ya jeshi hilo kwa umma kuwa hawataruhusu Serikali kuangukia mikononi mwa watu wasiojulikana.
“Jeshi letu halitaruhusu Serikali ya Sudan iangukie au kutereza kuelekea kwenye mikono ya watu wasiojulikana,” alisema.
Jenerali Maarouf alisema kuwa watu wanaoandamana kupinga Serikali ni wasaliti wa Taifa wanaoipaka tope taswira ya nchi hiyo.
Jeshi limetoa taarifa hiyo ikiwa ni siku chache tangu Rais Al-Bashir azuru Misri na nchi washirika, akitafuta msaada wa kuokoa uchumi wa nchi yake.
Waandamanaji walianza kufanya maandamano ya kupinga Serikali kufuatia tangazo la kupanda kwa bei ya mafuta pamoja na chakula.
Hivi karibuni, Rais Al-Bashir alisema kuwa hawezi kuachia madaraka kutokana na maandamano, bali kwa kupitia sanduku la kura au kulikabidhi jeshi.
Video: Ndugai amlipua Lissu, ambana Zitto
Al-Bashir ameiongoza nchi hiyo kwa kipindi cha takribani miaka 30 tangu alipoingia madarakani kupitia mapinduzi yasiyomwaga damu mwaka 1989.