Wanajeshi wa Niger wametangaza kumuondoa madarakani Rais wa Taifa hilo, Mohamed Bazoum ikiwa ni saa chache baada ya rais huyo kuzuiliwa ikulu na kikosi cha walinzi wa rais kinachoongozwa na Jenerali Omar Tchiani huku wakisema wamevunja katiba, kusimamisha taasisi zote na kufunga mipaka ya nchi.
Taarifa iliyosomwa na Kanali Amadou Abdramane kupitia Televisheni ya Taifa usiku wa kuamkia leo Julai 27, 2023, imeeleza kuwa vikosi vya ulinzi na usalama vimefikia hatua hiyo kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama, utawala mbovu, hali mbaya ya kiuchumi na kijamii.
Aidha, wametoa amri ya kutotoka nje nchi nzima, huduma katika taasisi zote za umma zimesitishwa, hadi hapo taarifa nyingine itakapotolewa huku wakionya kuhusu uingiliaji wowote ule wa kigeni, na kwamba wapo tayari kufanya mazungumzo na jumuia ya kitaifa na kimataifa.
Kwa sasa Rais huyo wa Niger, Mohamed Bazoum anashikiliwa na Wanajeshi wa kikosi cha walinzi wa rais katika ukanda huo ambao hata nchi mbili jirani, Mali na Burkina Faso, nazo zimekuwa zikikumbwa na mapinduzi yaliyochochewa na maasi ya makundi ya Jihadi katika miaka ya hivi karibuni.