Wakuu wa majeshi wa Jumuiya ya kikanda ya Afrika Magharibi – ECOWAS, wamekubaliana juu ya mpango wa uwezekano wa kuingilia kati kijeshi nchini Niger, baada ya viongozi wa mapinduzi kushindwa kurejesha utawala wa kiraia.
Wakuu hao wa Majeshi, walikutana kwa mazungumzo katika mji mkuu wa Nigeria wa Abuja, kujadili njia za kushughulikia mgogoro huo, uliokumba kanda ya Sahel tangu mwaka 2020.
Kamishna wa ECOWAS, Abdel-Fatau Musah amesema, vipengele vyote vya uwezekano wa uingiliaji kati vimefanyiwa kazi na vinajumuisha rasilimali zinazohitajika, namna gani na lini wanaweza kutuma wanajeshi.
Musah ameongeza kuwa Jumuiya hiyo ya kikanda inataka “diplomasia kufanya kazi” na kusema wanatuma ujumbe wa wazi kwa viongozi wa kijeshi kwamba wanawapatia fursa zote za kubatilisha kile walichokifanya.