Viongozi wa kijeshi wa Niger wametoa masaa 48 kwa mabalozi wa Ufaransa, Ujerumani, Nigeria na Marekani kuondoka nchini humo, hatua inayokuja wakati mvutano ukizidi kuongezeka kuhusu tishio la hatua za kijeshi kutoka kwa jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS.
Kupitia andiko la barua kwa serikali za nchi hizo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Niger imesema uamuzi huo umetokana na hatua ya Mabalozi wa nchi hizo kukataa mwaliko wa Serikali kwa ajili ya mkutano wa Ijumaa na hatua nyingine za Serikali zao kuwa kinyume na maslahi ya nchi yao.
Hata hivyo, Ubalozi wa Ufaransa nchini Niger umelikataa tangazo hilo ukisema kuwa Paris, hautambui mamlaka ya watawala wa kijeshi ambapo hatua ya maafisa hao ni ya hivi karibuni katika uhusiano unaozidi kuzorota kati ya utawala mpya wa Niger na mataifa kadhaa ya nchi za Magharibi, na ECOWAS.
Hata hivyo, Serikali ya Ufaransa imekuwa ikitoa wito wa mara kwa mara wa kuunga mkono wito wa ECOWAS wa kutaka kurejeshwa madarakani utawala wa kiraia uliopokwa kwa Rais wa Taifa hilo, Mohamed Bazoum, ambaye alipinduliwa Julai 26, 2023.