Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limefanya mabadiliko ya tozo za ukaguzi wa usalama dhidi ya majanga ya moto katika Majengo na maeneo mbalimbali pamoja na utaratibu wa ukusanyaji wa tozo hizo yaliyoanza rasmi Julai, 2022.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hii leo Agosti 11, 2022 jijini Dodoma na Msemaji wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Makao Makuu, SACF Puyo Nzalayaimisi amesema Tozo hizo zinakusanywa kwa mujibu Sheria namba 14 ya mwaka 2007 iliyoainisha mabadiliko hayo.
Amesema, “Napenda kuutaarifu umma kuwa, kuanzia mwezi Julai 2022 kumekuwa na mabadiliko na awali Jeshi lilibeba jukumu la kumfuata mteja na kuomba kufanya ukaguzi katika Jengo, eneo au chombo cha usafiri na utaratibu huu kwa sasa umeboreshwa zaidi ili kuliwezesha Jeshi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.”
Aidha, ameongeza kuwa kanuni tajwa ya ukaguzi na vyeti imeelekeza kuwa ni wajibu wa mteja au mmiliki wa jengo, eneo au chombo cha usafiri ambaye hajafanyiwa ukaguzi kufika ofisi za Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuomba kukaguliwa.
Nzalayaimisi amesema, kwa mujibu wa kanuni hiyo ni wajibu wa mteja kufika katika vituo na Ofisi za Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika mikoa yao ili waweze kuweka mpango kazi wa kukaguliwa wakati Jeshi hilo likiendelea kuboresha mifumo ili wananchi na taasisi zote waweze kuomba kupitia mtandao.
Ameongeza kuwa, “Tunaujulisha umma mabadiliko ya gharama za tozo katika maeneo mengi kama vile maduka, viwanda, makazi, ofisi, shule, nyumba za kuishi, usomaji wa ramani pamoja na gharama za usajili wa makampuni yanayojishughulisha na utoaji huduma za kuuza vifaa, uwekaji wa vifaa vya kuzima moto pamoja na mifumo ya uzimaji moto.
Balozi Sokoine aongoza ujumbe wa Tanzania maandalizi mkutano wa SADC