Jezi tatu tofauti zilizovaliwa na Nahodha na Mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Argentina Lionel Messi wakati wa Fainali za Kombe la Dunia 2022, zitauzwa kwa njia ya mnada.
Messi mwenye umri wa miaka 36, alifanikiwa kutwaa Ubingwa wake wa kwanza wa Dunia akiwa na kikosi cha Argentina katika Fainali hizo zilizofanyika nchini Qatar.
Messi alicheza katika mechi zote saba za Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar, lakini jezi mbili pekee kati ya tatu ambazo Messi alivaa wakati wa hatua ya makundi ndizo zitauzwa kwa mnada, baada ya mshiriki wa kikosi cha Australia Cameron Devlin kubadilishana Mshambuliaji huyo wa zamani wa FC Barcelona wakati wa mchuano huo.
Jezi iliyovaliwa na Mshambuliaji huyo wakati wa mchezo wa Fainali dhidi ya Ufaransa inatarajiwa kuuzwa zaidi ua Pauni Milioni 8, katika mnada maalum utakaoondeshwa na kampuni ya Sotheby mjini New York nchini Marekani.
Rekodi pekee ya mauzo ya jezi ya Argentina iliopo kwa sasa ni ile iliyowekwa baada ya mauzo ya Jezi ya Gwiji wa soka wa nchi hiyo Diego Maradona, ambayo aliivaa kwenye mchezo dhidi ya England mwaka 1986 na kufunga bao la Mkono wa Mungu.
Jezi ya Gwiji huyo ilipigwa mnada mwaka 2022 kwa mauzo ya Pauni Milioni 7.1.
Kiongozi Mkuu wa Kampuni ya mnada ya Sotheby Brahm Wachter, amesema uuzaji wa Jezi sita za Messi “unasimama kama tukio kubwa katika historia ya mnada”.
“Kombe la Dunia la FIFA la 2022 linasimama kama moja ya matukio makubwa zaidi katika historia ya michezo, yanayohusiana sana na safari ya ushujaa ya Messi na kuweka hadhi yake kama mchezaji bora zaidi wa wakati wote,” Wachter amesema.
Messi ambaye ni mshindi mara nane wa Ballon d’Or, amekuwa mchezaji wa kwanza katika historia ya Kombe la Dunia kufunga katika hatua ya makundi, 16 bora, Robo Fainali, Nusu Fainali na Fainali ya Michuano hiyo.
Wachter ameongeza: “Ni heshima kwa ‘Sotheby’s kuwasilisha na kuonyesha maudhui haya ya thamani sana kwa umma, ambayo yanajumuisha uzuri kamili wa mchezaji ambaye amefafanua upya mipaka ya ubora wa soka.”
“Sehemu ya mapato ya mnada huo yatatolewa kwa Mradi wa Unicas, unaoongozwa na Hospitali ya Watoto ya Sant Joan de Deu (SJD) Barcelona kwa msaada wa Leo Messi, ili kukidhi mahitaji ya watoto wanaougua magonjwa adimu.”
Jezi za Messi zitaonekana katika makao makuu ya ‘Sotheby’ New York katika maonyesho ya bure, ya umma wakati wa mchakato wa zabuni, ambayo itafunguliwa kati ya 30 Novemba na 14 Desemba.