Mastaa wa Ligi Kuu ya England wameziambia klabu zao kwamba watafurahi endapo watavaa jezi zilizopachikwa kamera kifuani kwenye kila mechi.
Aidha mapendekezo hayo yatapigwa chini kwa sababu sheria ya IFAB hairuhusu mfumo huo wa kamera kutumika kwenye mechi za ushindani.
Mapendekezo hayo ni baada ya mchezaji wa Newcastle kiungo, Bruno Guimaraes ambaye alivaa jezi ikiwa na kamera wakati wa mechi ya kirafiki dhidi ya Aston Villa iliyochezwa Philadelphia, Marekani wikiendi iliyopita na mchezo huo ukamalizika kwa sare ya mabao 3-3.
Naye mchezaji wa Villa, Youri Tielemans alivaa jezi iliyopachikwa kamera kifuani yenye uwezo wa kurekodi matukio kwa lenzi.
Hata marefa waliochezesha mchezo huo walivalia jezi zilizopachikwa kamera kifuani jambo ambalo lilileta kivutio na ushawishi kwenye mashindano mengine.
Chanzo cha habari kimeripoti endapo itakubaliwa itabadilisha mabadiliko ya sheria ya mchezo wa soka kama klabu zitaruhusu mfumo huo.
Bodi za ligi zimekuwa zikifanya kazi na kampuni kutoka Israel ili kuzipa fursa klabu ya kutumia mfumo huo kwa mujibu wa ripoti.