Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimekanusha kukiuka sheria ya vyama vya siasa kama ambavyo barua kutoka kwa msajili wa vyama vya siasa nchini inavyoeleza.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo Oktoba 3, 2019 na mkuu wa idara ya mawasiliano ya chama hicho Tumaini Makene, chama kimekiri kupokea taarifa hiyo lakini wamesema Katiba ya chama hicho inatoa mamlaka kwa kamati, kusogeza mbele uchaguzi mkuu ndani ya chama.

” Tarehe ya uchaguzi mkuu wa chama, inaweza kurekabishwa kwa kusogezwa mbele kwa muda usiozidi mwaka mmoja, toka mwisho wa uhalali wa uongozi uliopo, mamlaka ya kufanya marekebisho haya yameachwa kwa kamati kuu” imeeleza taarifa hiyo.

Kwamujibu wa taarifa hiyo, Kamati kuu ya chama hicho, ilikaa katika kikao chake cha tarehe 27 na 28, Julai, 2019 na kurekebisha ratiba ya uchaguzi, ambapo utakamilika mwezi Disemba kwa ngazi ya taifa na kwamba kwasasa kinaifanyia kazi barua hiyo ili iweze kuifikia Ofisi ya msajili wa vyama vya Siasa ndani ya muda husika.

Awali ofisi ya msajili wa vyama vya siasa nchini, ilitoa taarifa kuwa uongozi wa chama hicho chini ya Mwenyekiti wake Freeman Mbowe, umemaliza muda wake tangu Septemba 14, 2019 na kukitaka kuandika maelezo ya kwanini kisichukuliwe hatua baada ya kukiuka Sheria ya vyama vya siasa na kuwataka wawasilishe maelezo hayo Oktoba 7 mwaka huu, majira ya saa 9:30 jioni.

Ngorongoro Heroes kuikabili Kenya kesho
RC Chalamila awasimamisha shule wanafunzi wote kidato cha 5 na 6