Yanayotokea kweye mitandao ya kijamii, ndicho alichofikiria mtu aliyebuni na kuanzisha jukwaa hilo linalowakutanisha watu wa kariba mbalimbali kutoka kila pembe ya dunia.
Mitandao ya kijamii imekuwa ni sehemu ya fursa kwa watu wengi na wapo wanaoitumia mitandao hii ili kufanya biashara na kufanikisha shughuli mbalimbali.
Uwanja wa Wanawake umeona mengi yanaendelea katika mitandao ya kijamii na kwa upande wa Instagram mtandao huu umegeuzwa kama Mahakama au sehemu ya kupatia haki na huruma kutoka kwa wengine.
Hapo awali, matataizo ya ndani au yanayohusu familia yalikuwa yakijadiliwa katika vikao vya familia, Serikali za Mitaa, Ustawi wa jamii au Mahakani, lakini siku hizi mambo yamekuwa tofauti kwani kila kitu utakikuta Instagram yenye Mawakili, Mahakimu na washauri.
Wanawake ndiyo wamekuwa vinara wa kutoa taarifa zao huku wakiamini mitandaoni ndiko watapata ushauri huruma na haki, wakisahau kufanya hivyo ni kuzidi kujiaibisha, maana hata wasiojua watalazimika kujua kuhusu yanayowakabili.
Inapotokea wapenzi au wanandoa wameachana na labda walijaliwa watoto au mtoto basi uhusiano wao utaendelea kuwepo kwa ajili ya malezi ya watoto, kiustaarabu inaminika kuwa watu hawa ni wazazi basi watakuwa na namna ya kuwasiliana kama si wao moja kwa moja, basi hata kutumia watu wengine ndani ya familia.
Aidha, inapotokea kushindikana katika hilo basi Mahakama, Ustawi wa Jamii vinaingia kuhakikisha kutengana kwa wazazi hakuleti athari katika ukuaji na ustawi wa watoto.
Lakini hayo yote siku hizi yameachwa mama hajapewa matunzo ya mtoto anapeleka kesi instagram, baba hajanunua nguo za sikuku au kulipa ada malalamiko atayakuta mtandaoni, mama ataandika waraka huku akimnanga mzazi mwezie akieleza namna anavyoshindwa kutekeleza majukumu yake kwa mtoto au watoto wake, Swali ni je haya yanafanyika kwa faida ya nani?
Hata hivyo, wapo wanaoweka hadi risiti za gharama wanazotumia kuwatunza watoto wao ili kuudhibitishia umma kuwa baba hatimizi majukumu yake.
Ustaarabu huja pale baba anapoamua kunyamaza, lakini ikitokea baba mwenyewe anahitaji huruma ya wananchi basi kila kitu kitaanikwa mtandaoni, lakini ukweli ni kwamba ustawi wa mtoto malezi ya mtoto yanapaswa kuwa kwenye ngazi ya familia sio umma wa Instagram.
Wenye tabi hizi wanapaswa kuacha na hata kama unafikiri kufanya usijaribu, kwa kuwa haina tija na akama umeamua kuwa na maisha yako ama mmekubaliana kila mmoja awe na maisha yake basi iwe hivyo kwa amani shirikianeni kwenye malezi bila kuhusisha mitandao na ikitokea imeshindika sheria zifuatwe.
Ni aibu kwa mwanamke wa kisasa kulilia matunzo ya mtoto mtandaoni, sheria iko macho katika kuhakikisha kuwa mtoto anapata malezi bora ni wewe kuamua kufuata mkondo huo au kunyamaza kimya na kupambana na katika jitihada zako kumuwezesha mtoto au watoto wako kuishi.
Siku hizi wawanawake wanajitafutia kama unaweza kupata fedha ya kuweka kifushi kila siku ili uingie mtandaoni basi itumie hiyo kama fursa ya kukuwezesha kupata shughuli ya kukuingizia kipato.